waja-schools

Afisa Afya Wilaya ya Mbogwe afikishwa Mahakamani kwa madai ya kuomba na kupokea rushwa

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Geita imemfikisha mahakamani Edward Mahugija ambaye ni Afisa Afya katika Wilaya ya Mbogwe kwa makosa ya kuomba na kupokea rushwa na kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu.

Mshitakiwa amefikishwa mahakamani Februari 23, 2017 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Bukombe Mhe Gabriel Kurwijila ambapo alisomewa mashitaka na mwaendesha mashitaka wa TAKUKURU Bi. Husna Kiboko.

Mwendesha mashitaka aliieleza Mahakama kwamba Octoba, 2017 katika Wilaya ya Mbogwe mshitakiwa alitenda kosa kinyume na kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya mwaka 2007. Kwamba mshitakiwa aliomba na kupokea rushwa Tsh 390,000.00 (laki tatu na tisini tu) kutoka kwa wafanyabiashara ili aweze kuwarudishia funguo baada ya kufunga sehemu zao za biashara.

Ilielezwa kuwa, mshitakiwa pia alitenda kosa la kujipatia kiasi hicho cha fedha kwa njia za udanganyifu kinyume na Kifungu cha 302 cha Kanuni ya Adhabu. Kwamba, mshitakiwa alipokea fedha kutoka kwa wafanyabiashara akidai ni faini baada ya kufunga biashara zao na kuwaandikia ilani ya kufunga biashara. Hata hivyo hakuwapatia risiti wala kuwasilisha fedha hiyo kwa mwajiri wake.

Mshitakiwa alikana mashitaka na Upande wa Mashitaka uliieleza Mahakama kuwa uchunguzi umekamilika na uko tayari kwa ajili ya usikilizwaji wa hoja za awali kwa tarehe ambayo ingepangwa na Mahakama na haukuwa na pingamizi dhidi ya dhamana yake.

Mshitakiwa yuko nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana ambayo ni kuwa na wadhamini wawili wenye mali isiyohamishika yenye thamani isiyopungua Tsh 4,000,000.00. Kesi imehairishwa hadi itakapokuja kwa ajili ya mshitakiwa kusomewa maelezo ya awali.

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Geita Bw. THOBIAS NDARO ametoa shukrani kwa raia wema wanaotoa taarifa za rushwa kwa TAKUKURU.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *