waja-schools

GGM yakabidhi Mradi wa Bilioni 2.6 kwenye Halmashauri ya Mji wa Geita

Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) umekabidhi rasmi Mradi wa Maendeleo ya Uchumi wa Geita wenye thamani ya Shilingi Bilioni 2.6 kwenye Halmashauri ya Mji wa Geita. Mradi huo ulioanzishwa mwaka 2015 hukusanya  pamoja wajasiriamali kwenye eneo la Magogo Mjini Geita ukihusisha ufundi na ubunifu kwenye ufyatuaji wa tofali za kisasa, kudarizi na ushonaji nguo, utengenezaji wa mikanda na viatu.

Akizungumza kwenye tukio la utilianaji saini ya Makabidhiano ya Mradi huo yaliyofanyika kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mkurugenzi Mtendaji wa GGML Bw Richard Jordinson amesema kuwa Kampuni yake inajivunia kuwa mdau mkubwa wa Maendeleo ndani ya Mkoa wa Geita wenye Halmashauri mbili za Wilaya na Mji wa Geita.

“Dhamira yetu siku zote imekuwa kuanzisha Miradi endelevu yenye tija na inayozalisha Ajira kwa maendeleo ya Wananchi wanaozunguka eneo tunalofanyia shughuli zetu.Tunafurahi kwamba Miradi yetu inapoanza tu kutoa matokeo chanya,huwa tunaikabidhi rasmi Serikalini ili iweze kusimamiwa vizuri na kuleta tija iliyokusudiwa,”alisema Bw Jordinson.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita Mhandisi Modest Apolinary amesema kuwa Mradi huo sasa utaanza kutekelezwa rasmi kulingana na makubaliano yaliyoyofanywa baina ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) pamoja na Halmashauri ya Mji wa Geita.

“Kuna marekebisho kidogo tutayafanya wakati wa kutekeleza Mradi huu utakaokuwa unajishughulisha na kukuza ubunifu na ufundi kwa vijana wenye lengo la kujiajiri.Eneo la Magogo ambapo Mradi huo unatekelezwa litakuwa sasa ni kituo cha Mafunzo ambapo Vijana wetu mbalimbali watapatiwa ujuzi na ufundi na baada ya kuhitimu wataondoka na kuwapisha vijana wengine wapate fursa hiyo kwa maendeleo ya Halmashauri zetu,”alisema Mhandisi Apolinary na kuongeza kuwa Mradi huo hautaendeshwa tena na Vyama vya Ushirika na hautahusisha tena kitengo cha uchomeleaji.

Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel Luhumbi ameupongeza Mgodi wa Dhahabu Geita (GGML) pamoja na Halmashauri ya Mji wa Geita kwa kuwa na nyaraka inayowaongoza wakati wa makabidhiano ya Mradi huo.

“Tunapenda Mkoa wa Geita uwe na Miradi mingi endelevu na yenye tija lakini Miradi hiyo ni lazima iwe na kumbukumbu na nyaraka zitakatoa mwongozo na mweleko wa utekelezaji wa Miradi husika.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita ambae pia ndie Mstahiki Meya wa Hamashauri wa Mji huo Bw Leonard Bugomola amepongeza hatua ya Mgodi wa Dhahabu Geita (GGML) kukabidhi Mradi huo kwa vile anaamini utasaidia Dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Pombe Magufuli kuhamasisha ukuaji wa Viwanda kwenye Halmashauri.

Mgodi wa Geita umetekeleza miradi mingine mingi katika mkoa wa Geita katika nyanja za Elimu, Afya, Maji na Miundombinu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *