waja-schools

Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) waleta Matumaini na Tabasamu kupitia Ufadhili wa Upasuaji wa Midomo Sungura

17 April 2018,Mgodi wa Dhahabu wa Geita(GGM) kwa kushirikiana na Taasisi ya Rafiki Surgical Mission ya nchini Australia pamoja na Serikali wamezindua awamu ya kwanza ya Kampeni ya Upasuaji wa Midomo Sungura  kwa mwaka 2018 kwa kufadhili matibabu ya Watu 25 kwenye Hospitali ya Sekou Toure jijini Mwanza.

Hafla ya kuwaaga Wagonjwa hao ilifanyika katika Kituo cha Upimaji na utoaji Ushauri nasaha kinachofadhiliwa na Mgodi wa Dhahabu Geita mjini Geita ambapo wagonjwa wa Midomo Sungura pamoja na Familia zao walihudhuria.

Akiwapongeza Wazazi kwa kuwapeleka watoto kwenye zoezi hilo,Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Herman Kapufi alisema kuwa kumekuwepo na dhana potofu kuwa midomo Sungura ni laana na wagonjwa wake hawapaswi kusaidiwa.

“Nawapongeza wazazi na walezi wote waliofika kwenye huduma hii.Nawahimiza wazazi na walezi wengine pia wenye watoto wenye ulemavu kama huu wawasiliane na GGM katika kutafuta matibabu kwani midomo Sungura inatibika.Haipendezi kuwaficha watoto hawa nyumbani.Naihimiza jamii yote ya Geita iache kubagua watoto wenye ulemavu kama huu,”alisema Mh Kapufi akiishukuru GGM na Rafiki Surgical Mission pamoja na Serikali wanaoshirikiana kutoa huduma hiyo

Kaimu Mkurugezi Mtendaji wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita Bw Wayne Louw (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wagonjwa wa Midomo Sungura pamoja na  familia zao katika uzinduzi wa awamu ya Kwanza ya Kampeni ya Upasuaji wa Midomo Sungura unaofanywa na Mgodi wa Dhahabu Geita(GGM), pamoja naye ni  Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Herman Kapufi na wafanyakazi wa GGM

Akizungumzia Kampeni hiyo,Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa GGM Bw. Wayne Louw amesema kuwa kwa miaka 16 Mfululizo,GGM imekuwa ikichangia huduma hiyo na mpaka hivi sasa watu 1637 wamenufaika na huduma hiyo.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (Katikati) akizungumza katika uzinduzi wa mpango wa upasuaji wa Midomo Sungura. Pembeni ni Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Herman Kapufi (Kulia) na Meneja Mkuu wa Afya, Usalama, Mazingira na Mafunzo (HSE & T) Dkt . Kiva Mvungi (Kushoto).

“Tunajivunia kushiriki katika mpango huu na tutaendelea kutoa usaidizi kwa jamii inayotuzunguka.Tunawatakia wagonjwa wote kila la kheri na maisha mema baada ya upasuaji,” Alisema Bw. Louw

Akizungumza katika uzinduzi huo, Meneja wa Afya, Usalama, Mazingira na Mafunzo wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita Dkt. Kiva Mvungi alisema kuwa ulemavu wa Midomo Sungura ni moja kati ya matatizo makubwa yanayowakumba watu waliozunguka Ziwa Victoria, ambapo Mgodi upo.

“GGM kwa kushirikiana na Rafiki Surgical Mission pamoja na Serikali na wadau wengine, imejituma kusaidia watoto na watu wazima kwenye mkoa wa Geita wanaosumbuliwa na Midomo Sungura kwa kuwapatia matibabu ya upasuaji wa bure ili waweze kuwa na tabasamu mpya na matumaini mapya.

Awamu ya kwanza ya mpango huo imeanza Tarehe 15 Aprili 2018, ambapo GGM imedhamiria kufadhili watoto na watu wazima 25 wenye ulemavu wa Midomo Sungura kutoka vijiji tofauti mkoani Geita, ikiwemo utoaji wa malazi na chakula katika kipindi chote cha majuma mawili ya mpango huo unaofanyika Sekou Toure Hospitali, Mwanza,” alisema Dkt Mvungi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *